Story by Our Correspondents –
Rais Uhuru Kenyatta amefanya mabadiliko kadhaa katika baadhi ya mawaziri na makatibu nchini ili kuhakikisha wanawajibikia majukumu yao vyema katika kuwahudumia wananchi wote.
Akitangaza mabadiliko hayo, Msemaji wa Ikulu ya Rais Kanze Dena Mararo amesema Waziri wa Ugatuzi nchini Eugine Wamalwa amehamishiwa Wizara ya Ulinzi ili kushikilia nafasi ya Balozi Monica Juma aliyehamishwa Wizara ya Kawi.
Waziri wa Kawi nchini Charles Keter amehamishiwa Wizara ya Ugatuzi nchini huku Waziri wa Jinsia na huduma za umma Margaret Kobia akiongezewa majukumu zaidi na kuwa Waziri wa huduma za umma, jinsia, maswala ya kijamii na mipango maalum.
Hata hivyo Meja mstaafu Gordon Kihalangwa atakuwa Katibu katika Wizara ya Kawi, Mhandisi Dkt Joseph Njoroge atakuwa Katibu katika idara ya uchukuzi, Solomon Kitugo atakuwa Katibu katika idara ya ujenzi wa umma na Nelson Marwa akiwa Katibu katika idara ya ulinzi maalum, maswala ya kijamii na mipango maalum.
Hata hivyo Bi Kanze amesema ofisi ya Rais imechukua uamuzi wa kufanya mabadiliko hayo kwa kuzingatia kipengele cha 155 sehemu ya 5{a} na sehemu ya 4 ya Katiba ya nchi na kutekeleza mabadiliko hayo ambayo yameanza mara moja.