Picha kwa hisani –
Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi, amefanya mkutano na viongozi mbalimbali ikiwemo wa bunge la Seneti ili kujadili swala tata la ugavi wa mapato kwa serikali za kaunti.
Mkutano huo ambao umehudhuriwa na Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana nchini Wycliffe Oparanya, Kiongozi wa nchi ameahidi kuwa serikali itatoa shilingi bilioni 50 za ziada kwa kaunti katika juhudi za kuimarisha ugatuzi.
Rais Kenyatta amesema hatua hiyo itategemea kuimarika kwa uchumi wa nchi katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 huku akiwahimiza Maseneta kuafikiana kuhusu mvutano wa ugavi wa raslimali kwa kaunti.
Bunge la Seneti liliwakilishwa na Kiongozi wa wengi Samuel Poghisio, Kinara wa wengi katika bunge hilo Irungu Kang’ata, Seneta wa Siaya James Orengo aliye Kiongozi wa wachache bungeni humo miongoni mwa viongozi wengine.