Kwa mara nyingine tena, Wanawake wa mrengo wa ‘Embrace’ nchini wamepinga mswada unaonuia kuifanyia marekebisho katiba wa ‘Punguza mizigo’.
Wakiongozwa na Mbunge wa Likoni Bi Mishi Mboko, Wanawake waliyokongamana katika uwanja wa Tononoka Kaunti ya Mombasa hii leo, wameutaja mswada huo kama unaolenga kuwabandua nje ya uongozi akina mama humu nchini.
Kulingana na Mboko, Kenya ingali chini mno katika maswala ya uwakilishi wa wanawake katika nyanja mbalimbali za uongozi na hususan katika bunge la kitaifa hali inayostahili kubadilishwa.
Mboko amewataka Wakenya kusubiri ripoti ya jopo maalum la ‘Building Bridges Initiative-BBI’ kabla ya mwelekeo kutolewa kuhusu kuirekebisha katiba na wala wasiongozwe na maslahi ya kibinafsi ya kisiasa.
Katika mswada huo ambao unaendelea kujadiliwa katika mabunge ya Kaunti kote nchini unalenga kupunguza idadi ya wabunge kutoka 416 hadi 147 na iwapo mabunge 24 ya Kaunti kati ya 47 yataujadili na kuupitisha, basi bunge la kitaifa huenda likatoa mwelekeo wa kuwepo na kura ya maamuzi kuihusu katiba.