Picha kwa hisani –
Nyanja ya filamu nchini Kenya inaomboleza kifo cha muigizaji wenye kipawa Pretty Mutave. Mutave anafahamika kwa uigizaji wake katika vipindi kadhaa vya runinga ikiwemo Moyo (Waridi), Aziza (Dee), Maza (Zari), Arosto (Zelda), Udhalimu (Ashina) na Kijakazi (Lena).
Habari kuhusu kifo chake ilitangazwa na mwanahabari Lulu Hassan ambaye alimuomboleza akikumbuka jinsi walikuwa na mipango na mipango mikubwa pamoja lakini Mungu alikuwa amepanga tofauti.
“Tulikuwa na mipango lakini Mungu alikuwa na mipango bora… Lala salama. Lala na malaika Pretty. Inallilahi wa ina illayhi Rajiun.” – aliandika Lulu.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Rashid Abdalla, alikumbuka namna Pretty alikuwa mwingi wa furaha siku tano zilizopita wakati walikuwa wanashughulikia mradi Fulani.
“Siku tano zilizopita tulikuwa tunashughulikia mradi Fulani ambao uliundwa na wewe @iamibrach. Ulifurahia sana mradi huo. Nafikiri hii ndio ilikuwa njia ya kutuaga. Tutakukosa sana. Ulijitolea 100% ukiwa kazini. Safiri salama Pretty” – aliandika Rashid.
Kulingana na ujumbe wa Frank254 kwenye ukurasa wake wa Facebook, muigizaji huyo aliaga dunia akielekea katika hospitali moja mjini Mombasa. Frank pia alisema familia yake ilifichua kuwa mrembohuyo amekuwa akiugua tangu mwezi Machi mwaka huu.