Picha kwa hisani –
Maafisa wa polisi katika eneo la Likoni kaunti ya Mombasa wanawazuiliwa wanachama 11 wa kundi lililoharamisha la Mombasa Republican Council, MRC.
Afisa mkuu wa idara ya upelelezi katika gatuzi hilo dogo la Likoni Richard Koywer amesema 11 hao wameshikwa katika mtaa wa Maweni eneo la Likoni wakiendeleza mkutano wao kisiri bila hata ya kuzingatia masharti ya kudhibiti virusi vya Corona.
Richard amehoji kuwa kundi hilo la MRC liliharamishwa na Mahakama ya Mombasa yapata miaka 8 iliyopita na idara ya usalama katika eneo hilo haiwezi kuruhusu vikao vya aina yoyote ile ya kundi hilo.
Amesema polisi katika oparesheni yao ya kiusalama mwendo wa saa saba mchana wa leo wamelinasa kundi hilo lililo na wanachama wa kati ya umri wa miaka 34 na 68 wote wakiwa na vitambulisho maalum vya kundi hilo la MRC.
Washukiwa wote watazidi kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Likoni wakisubiri kufikishwa Mahakamani siku ya Jumatatu juma lijalo.