Story by Janet Shume-
Chama cha maafisa wa polisi waliostaafu nchini NAPOK tawi la kaunti ya Kwale kimewataka wakaazi wa kaunti hiyo kutowatenga maafisa wa polisi baada ya kustaafu katika jamii.
Phedilia Kisinyo mmoja wa wanachama katika chama hicho ambaye pia ni Kamishna wa polisi mtaafu, amesema maafisa wa polisi wamekuwa wakipitia madhila katika jamii baada ya kustaafu hali inayowaweka katika msongo wa mawazo.
Kisinyo amesema kupitia chama hicho cha wanachama 50 kwa sasa, wanalenga kuanzisha miradi mbalimbali itakayowanufaisha wanajamii pamoja na kujenga tena uhusiano kati ya maafisa hao wa polisi waliostaafu na jamii.
Akizungumza katika kikao cha kila mwezi katika majengo ya kituo cha polisi cha Kwale, Kisinyo amewataka maafisa wote wa polisi waliostaafu kujiunga na chama hicho ili kujumuika na maafisa wengine na kupata huduma mbalimbali ikiwemo ushauri nasaha.