Story by Gabriel Mwaganjoni –
Afisa mkuu wa polisi katika gatuzi dogo la Nyali katika kaunti ya Mombasa Daniel Masaba amesema idara ya usalama katika eneo hilo imewekeza pakubwa katika kuwashirikisha wakaazi kupambana na maambukizi ya virusi vya Corona.
Masaba amesema tangu mwaka uliyopita, wananchi wamewatazama polisi kama maadui hasa katika mikakati ya kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo, japo akahoji kwamba ni sharti wakaazi wazingatie kikamilifu masharti hayo.
Akizungumza katika kituo cha polisi cha Nyali, Masaba amesema polisi hawafai kulaumiwa kwani wanawakumbusha wananchi kuzingatia masharti na wala hawamuhangaishi yeyote kama wanavyodai baadhi ya wakaazi.
Kulingana na Masaba, ni sharti wakaazi watambue kwamba janga la Corona limeathiri watu wengi katika kaunti ya Mombasa hali inayomlazimu kila mmoja kuzingatia masharti ya kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo.