Story by Ali Chete –
Maafisa wa Polisi katika kaunti ya Mombasa wameidhinisha msako mkali dhidi ya majambazi waliyomuibia bunduki Kamanda wa Polisi wa kituo cha polisi cha Urban, George Kingi siku ya Jumatatu.
Afisa huyo aliibiwa bunduki hiyo iliyokuwa na risasi 15 alipokuwa akielekea nyumbani kwake mwendo wa saa nne usiku.
Kingi amesema majambazi watatu waliokuwa wamejihami kwa bastola na ambao walikuwa wameabiri tuktuk waliifunga barabara aliyokuwa akitumia kuendesha gari lake la binafsi na kisha kumuibia bunduki hiyo katika eneo la msikiti Ummu Khulthum mtaa wa Kizingo kaunti ya Mombasa kisha wakatoroka.
Hata hivyo Kamanda mkuu wa polisi Kanda ya Pwani Manase Musyoka amesema tayari msako mkali umeimarishwa dhidi ya majambazi hao kwani huenda wakatumia bastola ya Afisa huyo wa polisi kutekelezea uhalifu.