Maafisa wa usalama wametakiwa kuidhinisha uchunguzi wa kina kuhusu tetesi kwamba huenda magenge ya kihalifu ya ‘Wakali kwanza’ na ‘Wakali wao’ katika eneo la Kisauni Kaunti ya Mombasa yanaongozwa na wanasiasa.
Mkurugezi mkuu wa Shirika la utetezi wa haki za kibinadamu nchini Haki Afrika Hussein Khalid amesema tetesi hizo zimekuwepo kwa muda mrefu na ni sharti Maafisa wa polisi waliangazie kwa kina swala hilo na kuwaandama wahusika wote.
Akiwahutubia Wanahabari katika hospitali kuu ya rufaa ya Ukanda wa Pwani Mjini Mombasa hii leo, Khalid hata hivyo amesema swala la usalama katika eneo la Kisauni limekuwa tata mno na ni sharti idara ya usalama kulipatia kipau mbele.
Kulingana na Khalid, swala la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana wa eneo hilo la Kisauni na kwengineko katika Kaunti ya Mombasa limechangia pakubwa katika kudidimia kwa hali ya usalama katika Kaunti hiyo.
Kauli ya mtetezi huyo wa haki za kibinadamu inajiri huku Kamanda mkuu wa polisi Kaunti ya Mombasa Johnston Ipara akiweka wazi kwamba Polisi watalazimika kutumia nguvu kupita kiasi kuyaangamiza magenge ya kijambazi katika Gatuzi hilo dogo la Kisauni.