Story by Janet/Taalia:
Afisa mkuu wa kituo cha polisi cha Kwale Phillip Ngata amewahimiza maafisa wengine wa usalama katika vituo mbalimbali vya polisi kutumia fedha walizopewa na serikali kuboresha mazingira katika vituo hivyo.
Afisa huyo wa usalama amesema serikali imekuwa ikijitahidi kutenga fedha za kuboresha maisha ya maabusu hata kabla ya kufikishwa Mahakamani kwa kuhakikisha wanaishi katika mazingira bora pamoja na kula chakula kinachofaa.
Ngata amesisitiza kwamba washtakiwa pamoja na wafungwa gerezani wana haki sawa ya kuishi maisha bora licha ya wengine kuwa na makosa, akisema hali hiyo inaweza kuwasaidia katika kujirekebisha na kuwa watu wenye manufaa kwa jamii.
Akizungumzia eneo lake la kazi, Ngata ameahidi kuhakikisha maabusu wanaofikishwa katika kituo hicho wanapata mahitaji msingi, ikiwemo mahali pazuri pa kulala, chakula pamoja na mahitaji mengine msingi.