Picha kwa hisani –
Idara za usalama katika Kaunti za Kwale, Mombasa na Kilifi zimeungana ili kukabiliana na mchipuko wa kundi la ‘The Mombasa Republican Council’ (MRC ) katika Kaunti hizo tatu.
Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Gilbert Kitiyo amesema kundi hilo limeonekana kuchipuka upya na kutishia usalama wa Ukanda mzima wa Pwani.
Kitiyo amesema Idara ya usalama katika Ukanda wa Pwani haiwezi kulegezea kamba kundi hilo kwani athari zake za kiusalama zinafahamika vyema,akisema Maafisa wa usalama wako macho na watakabiliana watakaojiunga na kundi hilo.
Kitiyo amewataka wakaazi wa eneo la Pwani kutowaficha wanachama wa kundi hilo na badala yake wawafichue kwa Maafisa wa usalama ili wakabiliwe kisheria akisema zaidi ya wanachama 80 wa kundi hilo la MRC tayari wamehukumiwa na kufungwa gerezani.