Picha kwa hisani –
Police nchini Uganda wameizingira hoteli aliyoingia mgombea wa urais nchini humo Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine na maafisa wake wa kampeni,katika mji wa Hoima magharibi mwa Uganda.
Bobi ametuma ujumbe wake wa twitter akisema kuwa alilazimika kutumia njia ndefu kufika mjini humo baada ya wanajeshi kufunga barabara ambayo alitarajia kutumia.
Kulingana na vyombo vya habari nchini humo Bobi Wine alikuwa amekatazwa kuingia katika mji huo ambako alikuwa amealikwa kama mgeni katika kipindi cha redio.
Wagombea katika uchaguzi ujao katika taifa hilo wameamrishwa kufanya kampeni zao kwa njia ya vyombo vya habari na kuepuka mikusanyiko mikubwa ya watu kwasababu ya virusi vya corona.
Wiki iliyopita Bobi Wine alitiwa nguvuni kwa kukiuka sheria za kuzuwia virusi vya corona.