Idara ya usalama katika kaunti ya Mombasa ikishirikiana na Idara ya Afya katika kaunti hiyo inawasaka watu watano waliotoroka na familia zao baada ya kupimwa virusi vya Corona katika mtaa wa Old town na kupatikana wakiwa wameambukizwa.
Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho ameitaja tabia hiyo kama ya aibu, akisema watano hao watakaponaswa watatengwa na baadaye kufunguliwa mashtaka Mahakamani.
Joho amewahimiza wakaazi wa kaunti ya Mombasa kujitokeza na kupimwa kwa hiari ili kutoiweka kaunti hiyo katika hatari ya kusambaa kwa maambukizi ya Corona.
Kwa upande wa Idara ya Afya ya kaunti ya Mombasa, imeweka wazi kuwa japo kuna baadhi ya wakaazi wanaojitokeza kupimwa kwa hiari bado kuna changamoto ya kudhibiti maambukizi ya Corona.