Kamanda mkuu wa polisi kaunti ya Mombasa Johnston Ipara. Picha / Gabriel Mwaganjoni
Taarifa na Gabriel Mwaganjoni.
Likoni, Mombasa, Mei 22 – Idara ya usalama imesema kuwa maafisa wa usalama watatumia nguvu zaidi katika kuyakabili magenge ya kihalifu katika gatuzi dogo la Likoni, Kaunti ya Mombasa.
Kamanda mkuu wa polisi kaunti ya Mombasa Johnston Ipara amesema kwamba magenge hayo yamevuruga usalama katika eneo hilo na itawalazimu maafisa wa polisi kutumia nguvu kupita kiasi ili kuyasambaratisha .
Ipara amesema polisi hawalengi kuwapiga risasi na kuwauwa vijana wanaojihusisha na uhalifu, badala yake watakaonaswa katika operesheni hio watakabiliwa kisheria.
Ipara amesema kwamba jamii imewasihi maafisa wa polisi kuyakabili magenge hayo, huku akiitaka jamii na Viongozi wa kijamii mashinani kufanya kazi na idara hiyo ili kuudhibiti uhalifu.
Kauli ya Ipara inajiri baada ya visa vya uvamizi na mauaji kukithiri katika eneo hilo la Likoni.