Maafisa wa polisi katika eneo la Kaloleni kaunti ya Kilifi wamemtia nguvuni kijana mmoja aliyekuwa akisafirisha Mihadarati aina ya bangi iliokuwa na misokoti 5,231 katika mtaa wa Misufiini eneo la Mariakani.
Akithibitisha kunaswa kwa bangi hiyo, Afisa mkuu wa polisi eneo la Kaloleni Ezekiel Chepkwony amesema polisi walipashwa habari na wakaazi na wakamvua kijana aliyekuwa na bangi hiyo ya thamani ya zaidi ya shilingi milioni moja.
Chepkwony amewashauri wakaazi kuendelea kushirikiana na maafisa wa polisi katika juhudi za kukabiliana na mihadarati.
Kwa upande wake Mbunge wa Kaloleni Paul Katana amewashauri vijana katika eneo bunge hilo kutojihusisha na biashara hiyo haramu, akisema imewaangamiza vijana wengi.