Story by Gabriel Mwaganjoni:
Idara ya usalama katika kaunti ya Mombasa imebuni kamati maalum za kiusalama zinazowahusisha viongozi wa kijamii mashinani ili kudhibiti usalama katika gatuzi dogo la Kisauni na Nyali.
Kamishna wa kaunti ya Mombasa John Otieno amesema kamati hizo zina majukumu ya kufanya kazi bega kwa bega na maafisa wa polisi ili kuyazima megenge ya kihalifu katika maeneo hayo.
Akizungumza alipofanya vikao vya kiusalama katika maeneo hayo mawili, Otieno amesema kuwahusisha viongozi wa kijamii wakiwemo Wazee wa mitaa na Mabalozi wa nyumba kumi kutawawezesha wakaazi katika sehemu hizo kuwafichua wahalifu.
Wakati uo huo, amesema idara ya usalama katika kaunti hiyo imewekeza katika mipangilio ya usalama mashinani hasa msimu wa sherehe za krismasi na mwaka mpya unapowadia ili kuzuia uhalifu na kuondoa hofu.