Story by Our Correspondent:
Katibu katika Wizara ya usalama nchini Raymond Omollo amesema ujenzi wa amani na usalama wa kijamii ni lengo kuu kwa taifa hili na juhudi hizo zinahitaji mchango wa kila mmoja na wala sio maafisa wa usalama pekee.
Omollo amesema Wizara ya usalama nchini inaendeleza mikakati bora itakayochangia kuzuia migogoro ya vurugu na kushughulikia ipasavyo vitisho vya usalma nchini.
Akizungumza katika kikao cha kuangazia usalama wa taifa kulichohudhuriwa na wadau mbalimbali wa maswala ya usalama kutoka mataifa ya kigeni, Omollo amesema juhudi hizo zitafaulu kupitia usanifu mpya wa ujenzi wa amani.
Aidha amesisitiza umuhimu wa jamii kushirikiana na maafisa wa usalama katika kuzuia utovu wa usalama, akisema swala hilo litafaulu kwa kuhakikisha wananchi wanakumbatia kanuni za mazungumzo, upatanisho na kutotumia nguvu.
Kwa upande wake Mshirikishi wa baraza la umoja wa mataifa UN kuhusu amani na usalama, Stephen Jackson amesema baraza la umoja wa mataifa limejitolea kupiga jeki juhudi za serikali ya Kenya katika kuhakikisha amani na usalama unashuhudiwa kote nchini.