Story by Ephie Harusi –
Idara ya usalama kaunti ya Kilifi imewataka madereva wa magari ya uchukuzi wa umma, yale ya masafa marefu na kibinafsi kuwa makini zaidi barabarani ili kuepuka kushuhudiwa kwa ajali.
Kamishna wa kaunti ya Kilifi Kutswa Olaka amesema ongezeko la visa vya ajali ya barabarani imetokana na madereva kuendesha magari yao kwa mwendo wa kasi bila ya kuzingatia sheria za trafiki.
Olaka amesema maafisa wa trafiki katika kaunti ya Kilifi wataendeleza doria katika maeneo ya barabarani ili kuhakikisha wanaotumia barabara wanazingatia sheria za trafiki hasa msimu huu wa sherehe za krismas na mwaka mpya.
Hata hivyo amewataka wasimamizi wa Sacco za matatu katika kaunti hiyo kutowaajiri madereva wasio na maadili katika utendakazi wao, akidai kwamba wakati mwingi madereva hao huchangia kushuhudiwa kwa ajali za barabarani.
Kauli yake imejiri baada ya watu 6 kuaga dunia na wengine 25 kujeruhiwa vibaya katika ajali ya barabarni eneo la Roka kwenye barabara kuu ya Malindi-Kilifi siku ya Jumamosi.