Story by Mwanaamina Fakii –
Msemaji wa Serikali Kanali mstaafu Cyrus Oguna amesema serikali imetenga shilingi bilioni 1.2 kununua chakula ili kuwakidhi wakaazi wanaokabiliwa na upungufu wa chakula.
Akizungumza katika eneo la Silaloni kule Kinango kaunti ya Kwale wakati wa zoezi la ugavi wa chakula cha msaada kwa wakaazi walioathirika na baa la njaa, Oguna amesema hatua hiyo ya serikali itaendelezwa ili kukabiliana na hali hiyo.
Kwa upande wake Gavana wa Kwale Salim Mvurya amesema takriban wakaazi elfu 130 wanakabiliwa na baa la njaa katika kaunti ya Kwale huku akisisitiza haja ya kuidhinishwa mikakati mwafaka ya kukabiliana na hali hiyo.
Hata hivyo wakaazi wa eneo hilo wakiongozwa na Hashim Kazuma Randu amesema kwa sasa mifugo imefariki kufuatia kiangazi kikali huku wengine wakililia serikali kuwasaidia na maji ya matumizi.