Story by Gabriel Mwaganjoni –
Kinara wa Chama cha ODM Raila Odinga amewasili katika kaunti ya Mombasa tayari kwa kongamano la chama hicho siku ya Jumamosi mjini Mombasa.
Odinga amepokelewa na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Sharif Nassir katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Moi eneo la Changamwe huku Nassir akihoji kwamba malengo ya ziara ya Odinga eneo la Pwani ni kuimarisha mikakati ya chama hicho.
Nassir amesema chama cha ODM hakijatikisika kama wanavyodai wapinzani, akisema chama hicho kiko imara na kinalenga kuwabwaga wapinzani wake katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022.
Siku ya Alhamis, chama hicho kilimteua Mohamed Hamid kama Mwenyekiti wa chama hicho katika kaunti ya Mombasa baada ya kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti na Mwakilishi maalum wa bunge la kaunti ya Mombasa Mohammed Hatimy mwezi Oktoba mwaka uliyopita.