Story by Our Correspondents –
Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga amewaagiza wabunge ambao ni wanachama wa ODM kuwasilisha hoja bungeni itakayositisha usumbufu na unyanyasaji unaotendewa wavuvi katika bahari hindi ya kaunti ya Kwale na maafisa wa Kenya Coast Guards.
Odinga amesema tabia hiyo ni lazima ikomeshwe ili wavuvi waendeleze shughuli zao bila ya usumbufu wowote huku akidai kwamba ana mipango ya kuboresha uchumi wa nchi kupitia mpango wa uchumi samawati na kuwatengea vijana ajira.
Hata hivyo ameshikilia mpango wake wa kuhakikisha kila familia isiojiweza inapokea shilingi elfu sita kila mwezi kutoka kwa serikali punde tu atakapoingia Ikulu, akisema ni lazima swala la umaskini likomeshwe nchini.
Naye Seneta wa Kwale Isaac Juma Boi amemtaka Odinga kuingilia kati swala la mzozo wa ardhi katika kaunti ya Kwale pamoja na kusitisha usumbufu na unyanyasaji unaofanyiwa wavuvi katika bahari hindi ya kaunti ya Kwale.
Kwa upande wake Seneta wa Siaya James Orengo amemsuta Naibu Rais Dkt William Ruto akidai kwamba amekosa kufahamu maswala msingi katika serikali na kuendeleza ahadi za uongo.
Hata hivyo Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed, amesema tatizo sugu la mzozo wa ardhi katika ukanda wa Pwani litatatuliwa na Odinga pekee pindi atakapoingia Ikulu huku akiwaraia wakaazi wa Pwani kumuunga mkono Odinga.