Story by Gabriel Mwaganjoni-
Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga amesema ni lazima taifa lizingatie demokrasia ili kulinda haki ya kila mwananchi na kuwezesha taifa kuwa na amani.
Akizungumza katika kaunti ya Mombasa wakati wa kongamano la viongozi wa ODM pamoja na viongozi wa vyama vyengine kutoka kanda ya pwani, Odinga amesema demokrasia itasaidia kumaliza dhulma nyingi zinazowakabili wakenya.
Naye mbunge wa Likoni Bi Mishi Mboko aliyehudhuria kongamano hilo amesema Odinga ndiye atakayepeperusha bendera ya chama cha ODM katika kinyang’anyiro cha urais mwaka wa 2022 kwani ana ushawishi mkubwa katika siasa za taifa hili.
Kwa upande wake Mbunge wa Jomvu Badi Twalib amesema mikakati tayari imewekezwa ili kuhakikisha chama cha ODM kinachukua nafasi yake katika Ukanda wa Pwani.
Hata hivyo Mbunge wa Mvita Abdulswamad Sharif Nassir amefichua kwamba uongozi duni ulipo kwa sasa nchini unapaswa kuzimwa na ODM kuunda Serikali ijayo, kauli ambayo imeungwa mkono na Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho