Story by Our Correspondents
Mgombea wa kiti cha urais kupitia Muungano wa Azimio la umoja One Kenya Raila Odinga, amemteua Martha Karua kuwa mgombea mwenza wake.
Katika hotuba yake kwa taifa, Odinga amemsifu Karua akimtaja kama mwanamke aliyechangia mengi humu nchini hasa katika maswala ya sheria, kupigania demokrasia ya taifa na haki za wanawake sawa na kujitolea kwake kuliwajibikia taifa.
Odinga hata hivyo ametaja baadhi ya viongozi ambao watakuwa mawaziri katika baraza lake la Mawaziri iwapo ataingia Ikulu baada ya uchaguzi mkuu ambapo Peter Munya amepewa Wizara ya Kilimo, Ali Hassan Joho akapewa Wizara ya Ardhi, Kenneth Marende akapewa uspika wa bunge la Seneti miongoni mwa wengine.
Wakati uo huo amewataka wakenya kuunga mkono azma yake ya kuingia Ikulu huku akiwataka wapinzake wake wa kisiasa kuhakikisha wanafanya kampeni zao za uchaguzi mkuu kwa amani na wala sio siasa za vurugu.
Kwa upande wake mgombea mwenza wa Odinga Martha Karua amempongeza Odinga kwa kumpa nafasi hiyo huku akiwahimiza wafuasi wa Muungano wa azimio sawa na wakenya kuunga mkono safari yao ya kuingia Ikulu.
Hata hivyo Waziri wa Usalama wa ndani Dkt Fred Matiangi aliyehudhuria halfa hiyo katika maeneo ya ukumbi wa KICC, amepongeza uteuzi wa Martha Karua huku akiahidi kuwepo kwa usalama wa taifa wakati wa uchaguzi.