Story by Janet Shume-
Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga ameahidi kuwateua vijana katika baraza lake la mawaziri iwapo atachaguliwa kama rais wa taifa hili wakati wa uchaguzi mkuu ujao ili kuwajumuisha vijana katika uongozi.
Akizungumza katika Kongamano la vijana kutoka Mlima Kenya lililoandaliwa katika chuo kikuu cha Nairobi, Odinga amesema kuwapa nafasi za uongozi vijana ndio njia pekee ya kuboresha maendeleo hadi mashinani.
Odinga amesema analenga kuijumuisha jamii ya watu wanaoishi na ulemavu hasa vijana katika meza ya mazungumzo ili kupata uwakilishi sawa na kutatua changamoto mbalimbali zinazowasibu ikiwemo ukosefu wa ajira.
Akizungumza katika Kongamano hilo, Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho ambaye pia ni Naibu Kinara wa ODM, amewataka vijana kuwa na maono ya uongozi wa baadaye na swala hilo linaweza kuafikiwa iwapo watamuunga mkono Odinga.
Naye Katibu wa Chama cha ODM Edwin Sifuna amesisitiza kuwepo kwa serikali itakayojali maslahi ya wananchi kwa kuhakikisha wanajengwa uwezo sawia na kuwekeza mikakati ya kuhakikisha kuna kuwepo na usalama wa chakula.
Kwa upande wake Mshauri wa masuala ya vijana Jane Wangoi aliyezungumza kwa niamba ya vijana, imeweka wazi mipango ya maendeleo yaliotekelezwa na Odinga wakati akiwa Waziri mkuu huku akisema Odinga ana maono kwa vijana.