Story by Fatuma Rashid –
Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga ameahidi kufufua uchumi wa taifa hili iwapo wakenya watamchagua kama rais wakati wa uchaguzi mkuu wa Agosti 9.
Akiwahutubia wakaazi wa maeneo ya Maktau na Mwatate katika kaunti ya Taita taveta wakati wa mikutano ya kisiasa, Odinga amesema ana malengo ya kuhakikisha taifa hili linapiga hatua kimaendeleo.
Odinga hata hivyo ameshikilia msimamo wake wa kuwajenga uwezo vijana hasa kwa kuwabunia nafasi za ajira atakapoingia Ikulu huku akionekana kumsuta mpinzani wake wa kisiasa Naibu Rais Dkt William Ruto.
Odinga ameahidi kufanya mazungumzo na viongozi wa kaunti hiyo ikiwemo Gavana wa Taita taveta Granton Samboja, Mbunge wa Mwatate Andrew Mwadime miongoni mwa viongozi wengine waliotangaza nia zao za kuwania kiti cha ugavana wa kaunti hiyo.
Wakati uo huo amezindua mradi wa maji wa Nyangoro katika eneo la Maktau ili kuzikabili changamoto za ukosefu wa maji zilizokuwa zikiwakumba wakaazi wa eneo hilo.