Story by Ephie Harusi –
Mgombea wa kiti cha ugavana kaunti ya Kilifi kupitia chama cha KADU Asili Emmanuel Kombe Nzai amejiondo rasmi katika kinyang’anyiro hicho baada ya chama chake kuingia katika Muungano wa Kenya Kwanza.
Nzai amesema kutokana na uamuzi aliyouchukua sasa atajitosa mashinani kumpiga debe Aisha Jumwa aliyetangaza nia yake ya kuwania kiti hicho kupitia chama cha UDA huku akisema maswala ya wakaazi wa Pwani yatajumuisha katika meza ya serikali ya kitaifa.
Akizungumza na Wanahabari, Nzai amesema chama hicho kimefanya mazungumzo ya kina na Kinara wa chama cha UDA Dkt Rais William Ruto, kabla ya kuchukua hatua hiyo.
Haya yanajiri huku kaunti ya Kilifi ikitarajiwa kushuhudia kinyang’anyiro kikali cha ugavana mwezi Agosti 9 baina ya Mgombea wa kiti hicho kupitia chama cha PAA George Kithi, Aisha Jumwa wa UDA, Gedion Mung’aro wa ODM, miongoni mwa viongozi wengine.