Story by: Gabriel Mwaganjoni
Viongozi wa kisiasa na wale wa kijamii katika Wadi ya Kipevu eneo bunge Changamwe wamezindua hamasa kwa jamii kuhusu umuhimu wa kudumisha usafi wa mazingira katika maeneo wanayoishi.
Mwakilishi wa Wadi ya Kipevu Leila Nyanche amesema ni sharti wakaazi wafahamishwe kuhusu athari za uchafuzi wa mazingira na kutupa taka ovyo mitaani, ili wasilalamike pindi wanapotiwa nguvuni na kuadhibiwa kisheria.
Ni kauli iliyoungwa mkono na Afisa wa idara ya mazingira katika kaunti ya Mombasa Dan Makokha aliyesisitiza kwamba lengo kuu la vikao hivyo ni kuwafahamisha wakaazi kuhusu jukumu la kuyatunza mazingira.
Kwa upande wao wakaazi wa eneo hilo la Kipevu wameapa kutofufua majaa ya taka yaliofungwa rasmi na Serikali ya kaunti ya Mombasa na badala yake kushirikiana katika kudhibiti mirundiko ya taka katika maeneo ya makaazi.