Shirila la Ardhi la ‘Residents Land Protection Organisation of Kenya’limepinga vikali hatua ya Wizara ya ardhi nchini ya kuzisajili ardhi zote katika mtandao mmoja wa kidijitali.
Mwenyekiti wa Shirika hilo Dewelly Nyambu, amesema mpango huo unalenga kuwanyang’anya ardhi wananchi wa mashinani wasiokuwa na ufahamu wowote kuhusu maswala ya kidijitali.
Akizungumza katika eneo la Mtopanga kaunti ya Mombasa, Nyambu amesema hatua hiyo itazua utata katika umiliki wa ardhi hasa ikizingatiwa kwamba Waziri wa ardhi nchini Farida Karoney hakuchukua jukumu lolote la kuwaelimisha wananchi.
Wakati uo huo, ametaka mpango huo kusitishwa mara moja hadi pale wananchi watakapoelimishwa kuhusu utaratibu wote uliyotumika wa kuzisajili ardhi katika mtandao mmoja wa kidijitali ili kuzuia unyakuzi wa ardhi.