Kwa wapenzi wa mziki wa Bango kimekuwa kipindi kilichojawa na mshangao wa mara kwa mara pale msanii Elfarick Mandela maarufu kama Ricky Melodies anapoachilia kibao.
Vibao vyake hujawa na ucheshi na ujumbe unaokata umri wote. Hali inayowafanya watu wengi kuweza kuupenda mziki wake.
Kama ilivyo desturi yake mwaka huu Ricky ameweza kuachilia kazi nyingi ikiwemo kolabo kadhaa alizofanya na wasanii tajika na hata chipukizi katika mziki wa Bango. Wengi wetu tumekuwa tukitarajia mziki zaidi kutoka kwake ila hilo halitafanyika kwani msanii huyu amesalia na wimbo mmoja tu.
“Nataka niachilie nyimbo moja halafu nifunge mwaka, itakuwa ni kolabo na kiongozi wa Asili Band Jimmy Ngala. Siwezi kukwambia ni lini ila fahamu wakati wowote nitaachilia kazi mpya,” amesema Ricky.
Lakini Je ni kwa nini akaamua kufanya kolabo mwaka huu? Akijibu swali hilo Ricky amehoji kuwa kulikuwa na malalamiko mengi kuhusu kazi zake.
“Nimeachilia hits nyingi sana kama msanii pekee wa Bango na baadhi ya watu waliogopa sana jinsi nilivyokuwa nikiachilia mziki unaopenya. Nisingetaka kutengwa katika mziki ndio maana nimeanza harakati za kuwashirikisha wenzangu pia,” amesema Ricky.