Picha kwa hisani –
Mwanamuziki tajika kutoka Nigeria Ayodeji Balogun maarufu kama Wizkid ndiye mshindi wa mwaka huu wa kitengo cha msanii wa mwaka kwenye awamu ya 14 ya tuzo za “Headies” za taifa la Nigeria.
Alikuwa ameteuliwa kwenye kitengo hicho pamoja na wanamuziki kama vile Burna Boy, Davido, Tiwa Savage na Mayorkun. Hii ndiyo mara ya tatu anaibuka mshindi wa tuzo la msanii bora chini ya tuzo za Headies, kwanza alishinda mwaka 2012, akashinda mwaka 2016 na sasa ameshinda mwaka 2020.
Mwanamuziki huyo alisisimua mashabiki wake wengi ambao walikuwa wakihudhuria hafla ya kutuza washindi wa mwaka 2020 pale alipofika bila kutarajiwa kwani wasanii wengi wamekuwa wakisusia tuzo hizo miaka ya awali.
Wizkid alisafiri kutoka Ghana kwenda kushuhudia utuzaji wa washindi wa Headie jijini Lagos nchini Nigeria Jumapili tarehe 21 Februari mwaka huu.
Sherehe hiyo ambayo ilistahili kufanyika mwaka jana ilihairishwa hadi mwaka huu kutokana na janga la virusi vya Corona.
Wizkid alishinda pia tuzo la “Chaguo la watazamaji mwaka 2020” kwenye sherehe hiyo ya juzi. Mwaka 2019, mwanamuziki huyo aliandaa tamasha na kualika wanamuziki wengi katika eneo la 02 Arena, wakati tuzo hizo zikiendelea.