Story by Gabriel Mwaganjoni-
Mwakilishi wa Wadi ya Kadzandani kaunti ya Mombasa Fatuma Swaleh kwa jina maarufu Fatuma Kushe amemsihi Gavana wa kaunti hiyo Abdulswamad Sharif Nassir kuwapatia vijana wanaoshiriki mradi wa kuusafisha mji wa ‘Mombasa ni Yangu’ ajira za kudumu.
Kushe amesema mradi huo wa muda umewaondoa vijana katika maswala ya uhalifu na kukaa bure kwenye mabaraza, akisema kuwapatia vijana ajira za kudumu kutabadilisha maisha ya vijana hao na familia zao.
Akizungumza katika eneo la Bombolulu kaunti ya Mombasa wakati wa ziara ya Nassir ya kukagua mradi huo, Kushe amesema mradi huo unastahili kuwashirikisha akina mama wanaoishi katika viwango vya juu vya umaskini.
Kwa upande wake, Gavana Nassir amesema mradi huo ni wa kipekee kwani tayari umewawezesha vijana kuondoka kwenye maovu katika jamii, akihoji kwamba mradi huo utaendelezwa.