Story by Gabriel Mwaganjoni-
Tume ya kuajiri walimu nchini TSC itawapatia kipaumbele walimu wa shule za upili za viwango vya kadri yaani Junior Secondary katika zoezi la kuwajiri walimu mapema mwakani.
Hatua hii inajiri baada ya jopo lililoteuliwa kuangazia mfumo mpya wa elimu wa CBC kupendekeza kuajiriwa kwa takriban walimu elfu 30 wapya watakaofundisha wanafunzi watakaojiunga na shule hizo mwaka ujao.
Akizungumza katika kaunti ya Mombasa baada ya kushuhudia zoezi la ufunguzi wa nakala za mtihani wa kidato cha 4 KCSE katika gatuzi dogo la Nyali, Afisa mkuu mtendaji wa TSC Nancy Macharia amesema tayari wanakabiliwa na upungufu wa jumla ya walimu elfu 68 katika shule za upili kote nchini.
Nancy amesema TSC imekuwa ikiajiri walimu 5,000 kila mwaka akiongeza kwamba kuwaajiri walimu wapya 30,000 mwakani kutasaidia kuziba mwanya huo.
Mwezi Machi mwaka huu, serikali ilitangaza kutoa mafunzo kwa walimu elfu 60 kuhusu Mfumo mpya wa elimu -CBC kwa shule hizo japo zoezi hilo lililositishwa lakini sasa litaregelewa kwa kuzingatia wanafunzi wa Gredi ya saba.
Wakati uo huo amesema jumla ya watahiniwa 884,263 wanafanya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne kote nchini unaosimamiwa na Mameneja 10,416 sambamba na wasimamizi wengine 60,459.