Story by Gabriel Mwaganjoni-
Mgogoro umezuka kati ya mmiliki mmoja wa ardhi na wakaazi wa vijiji vya Kwa Noti na Moroto eneo la Jomvu-Mikanjuni, kaunti ya Mombasa baada ya wakaazi kudai kufungiwa barabara na mmiliki huyo.
Wakaazi hao wakiongozwa na George Okidi wamemtaka Gavana wa Mombasa Abdulswamad Sharif Nassir kuingilia kati na kuutanzua mgogoro huo.
Ni kauli iliyoungwa mkono na kiongozi wa vijiji hivyo, Dama Juma aliyelalamikia hatua hiyo akiitaja kuwa na athari ya moja kwa moja kwa jamii ya eneo hilo.
Kwa upande wao walimu katika shule za eneo hilo wakiongozwa na David Owino wamesema kufungwa kwa barabara hiyo kutaathiri shughuli za masomo kwani wanafunzi watalazimika kwenda mwendo mrefu ili kufika shuleni.
Hata hivyo, mmiliki wa ardhi hiyo Omar Ahmed amesema amekuwa akiishi kwenye ardhi hiyo na kwamba wema wake wa kuwaruhusu wakaazi hao kupitia kwenye makaazi yake umemponza.
Katika barua aliyoandikiwa Ahmed na msaidizi wa Naibu kamishna wa eneo la Miritini Margaret Ndoo, Ahmed aliamrishwa kusitisha shughuli zote za ujenzi katika eneo hilo hadi utata huo utanzuliwe.