Taarifa na Alphabet Mwadime.
Mzozo wa ardhi wa eneo la Kanamai huko Kikambala Kaunti ya Kilifi umechacha huku tukio la kupotezwa kwa vijana wawili katika hali tata likihusishwa na mzozo huo wa ardhi.
Mmoja wa waathiriwa hao Bi Beatrice Osino ameweka bayana kwamba Juma Said na Samuel Riango walitolewa kwenye matatu na kuingizwa katika gari la kibinafsi siku 11 zilizopita, hali ambayo imewatia hofu zaidi ya familia 471 zinaoishi katika ardhi hiyo inayokumbwa na mzozo ya ukubwa wa hekari 230.
Lamar Lugo, mkaazi wa eneo hilo na ambaye amelazimika kuishi msituni baada ya uvamizi na kufyatuliwa risasi nyakati za usiku na mchana na maafisa wa usalama amehoji kwamba maafisa wa polisi wanashirikiana na mwanasiasa huyo katika kuwahangaisha.
Katika mkao na wanahabari katika afisi za shirika la utetezi wa haki za kibinadamu nchini Haki Afrika mapema leo, Naibu mkurugenzi wa Shirika hilo Bi Salma Hemed amelitaja tukio hilo kama la kutisha na ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu.
Bi Hemed amesema kwamba lalama rasmi kuhusu swala hilo litawasilishwa kwa kiongozi mkuu wa mashtaka ya umma nchini Noordin Hajj na idara ya kuwalinda mashahidi hasa ikizingatiwa kwamba kesi hiyo ingali kotini ili kukomesha hali hiyo tata.
Mgogoro huo wa ardhi kati ya Mwanasiasa huyo na Wakaazi umedumu tangu mwaka wa 2014.