Story by Ephie Harusi:
Wakaazi wa kijiji cha Kuruwitu eneo la Shariani katika kaunti ya Kilifi wameachwa bila makao baada ya nyumba zao zaidi ya 20 kubomolea chini ya ulinzi mkali wa maafisa wa polisi.
Kulingana na wakaazi hao, ubomozi huo uliofanyika chini ya ulinzi mkali umesababisha watu wawili kupigwa risasi na kujeruhiwa vibaya.
Wakiongozwa na Hinzano Mumba na Douglas Thethe wakaazi hao wamesema ubomozi huo umefanyika kinyume cha sheria kwani hawakuwa wamepewa agizo lolote na Mahakamani.
Kwa upande wake Afisa wa maswala ya dharura katika Shirika la Haki Afika Alexander Mbela amekashfu vikali hatua hiyo akidai kwamba polisi hawafai kutumia nguvu kupita kiasi.
Naye Afisa wa Shirika la Kilifi Social Justice Centre Eric Mgoja, amekitaja kitendo hicho kama ukiukaji wa haki za binadamu huku akisema tayari wamewasilisha lalama zao kwa maafisa wa IPOA ili sheria ichukuliwe.
Hata hivyo Kamanda wa polisi kaunti ya Kilifi Nelson Taliti amesema kuna kundi la watu linalofahamika kama Team Mashamba ambalo huvamia mashamba ya watu na kuyauza.