Story by Gabriel Mwaganjoni –
Mwili wa mwanamume mmoja kwa jina la Mwinyi Mwinyi Mzungu aliyetiwa nguvuni na watu waliojitambulisha kama Maafisa wa polisi nyumbani kwake eneo la Utange kaunti ya Mombasa mwezi Disemba 20 mwaka uliyopita umepatikana katika makafani ya City uijini Nairobi.
Mkurugenzi mkuu wa Shirika la utetezi wa haki za kibinadamu la HAKI Afrika Hussein Khalid amesema mwili wa Mwinyi Mwinyi umetambuliwa na familia yake na Shirika hilo limekuwa likishirikiana na familia ya marehemu ili kuusafirisha mwili huo hadi nyumbani kwao Utange kwa mazishi.
Mwinyi Mwinyi alichukuliwa nyumbani kwake eneo la Utange mwezi Disemba mwaka uliyopita na hadi sasa familia yake imekuwa ikimtafuta katika vituo vya polisi na hifadhi za maiti katika hospitali mbalimbali kote nchini.
Kulingana na Shirika hilo, mwili wa Mwinyi Mwinyi ulikuwa na majeraha, ishara kamili kwamba aliteswa kabla ya kuuliwa kinyama.
Marehemu alikuwa mwandani wa karibu wa marehemu Bakari Masuo ambaye pia mwili wake ulipatikana katika hifadhi hiyo ya maiti ya City jijini Nairobi baada ya kutoweka katika njia tatanishi katika eneo la Mazeras kwenye barabara kuu ya Mombasa – Nairobi.