Maafisa wa uokoaji wameupata mwili wa mtu mmoja aliyehusika katika mkasa wa alfajiri ya leo ambapo gari dogo limetumbukia katika kivuko cha feri cha Likoni.
John Mutinda aliyekuwa na umri wa miaka 46 ameaga dunia baada ya gari walimokuwa wakisafiria kutoka upande wa Pwani kusini kuelekea Kisiwani Mombasa kutumbukia katika kivuko cha feri cha Likoni mwendo wa saa kumi na dakika ishirini hivi alfajiri ya leo.
Kulingana na taarifa kutoka kwa Kampuni ya huduma za feri nchini, dereva wa gari hilo ameamrishwa kusimama kwa kuwa tayari feri iliyokuwa imeegeshwa ilikuwa imeng’oa nanga kutoka upande wa Likoni kuelekea kisiwani japo akakaidi amri hiyo na kuliendesha gari hilo ndiposa likatumbukia katika Bahari hindi.
Haijabainika wazi gari hilo lilikuwa na watu wangapi ndani yake japo shughuli za kusaka watu wengine na gari hilo zinaendelea katika kivuko hicho.
Tukio hilo linajiri takriban miezi miwili tu baada ya mama na mwanawe kutumbukia katika kivuko hicho wakiwa ndani ya gari lao na wakaaga dunia.