Story by Our Correspondents –
Mwanariadha wa Kenya Agnes Jebet Tirop aliyeshinda medali ya shaba katika mbio za dunia za mita elfu 10 ameaga dunia.
Shirikisho la riadha nchini la Athletics Kenya limethibitisha kifo chake na kusema kwamba marehemu amekumbana na mauti yake baada ya kudungwa kisu na mumewe kufuatia ugomvi wa kifamilia.
Katika taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari shirika hilo limedai kumpoteza mwanariadha shupavu aliyeipa sifa taifa la Kenya kwa ushindi wake baada ya kuvunja rekodi za mbio za kilomita 10 za kinadada za Road to Records Race nchini Ujerumani na mbio za kinadada za Valencia Half Marathon.
Hata hivyo Tirop alishinda tuzo mbalimbali katika mashindano ya riadha mwaka wa 2013, 2014 na 2015 ikiwemo mashindano ya mbio za World Junior Cross Country mwaka wa 2013 nchini Poland.
Shirikisho hilo limesema polisi wameanzisha uchunguzi kubaini chanzo cha kifo chake.