Picha kwa hisani –
Mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 56 anauguza majeraha mabaya katika hospitali ya Mpeketoni Kaunti ya Lamu baada ya kushambuliwa na nyati akiwa shambani kwake.
Mwanamume huyo kwa jina Joseph Mwangi ameshambuliwa alipokuwa akilinda matikiti maji shambani mwake katika eneo la Ngoi huko Mpeketoni ambapo nyati huyo amemdunga pembe kifuani na tumboni na kumjeruhi vibaya.
Mwangi pia amejeruhiwa kichwani na wakaazi waliomuokoa kutoka kwa nyati huyo wamempata akivuja damu nyingi na tayari alikuwa amezirai.
Wakaazi wamelalamikia uvamizi wa mara kwa mara wa wanyama pori katika eneo hilo la Mpeketoni wakitaka Shirika la uhifadhi wa wanyamapori kuchukua hatua za dharura ili kuwalinda Wakaazi hao dhidi ya kushambuliwa na wanyamapori.
Wakaazi hao pia wamelalamikia mifugo wao kushambuliwa na chui na licha ya wao kuripoti kwa Shirika hilo la KWS, hakuna hatua zozote mwafaka zilizochukuliwa ili kuikabili hali hiyo.