Mahakama ya mjini Kwale imemuachilia kwa dhamana ya shilingi Milioni moja mwanamume mmoja aliyenaswa na vipande 12 vya pembe za ndovu vyenye thamani ya shilingi milioni 3.5 bila kibali.
Mahakama imeelezwa kwamba mnamo tarehe 17 mwezi aprili mwaka huu mwanamume huyo kwa jina Josphat Mtoi Kuri na wenzake ambao hawakuwa mahakamani alinaswa na pembe hizo zenye uzani wa kilo 35 katika hoteli ya Silent Logde eneo la Matuga kaunti ya Kwale akiwa anasubiri wateja wake.
Akiwa mbele ya hakimu Joe Omido mshukiwa amekana shitaka hilo na kuachiliwa kwa dhamana ya Shilingi milioni 1 na mdhamini wa kiasi sawa na hicho huku Kesi hiyo ikiratibiwa kutajwa tarehe 26 mwezi Aprili mwaka huu.
Kwenye ripoti iliyotolewa na maafisa wa shirika la KWS asubui ya leo kabla ya mshukiwa kufikishwa mahakamani imebainisha kwamba huenda mwanamume huyo alipata pembe hizo za ndovu katika ranchi Kiranze.