Story by Gabriel Mwagangoni –
Afisa mmoja wa kikosi cha kulinda mipaka BBU katika kaunti ya Lamu amejitokeza siku 17 baada ya kutoweka kufuatia tukio moja ambapo gari la wanajeshi lilikanyaga kilipuzi na kusababisha baadhi ya wanajeshi kufariki na wengine kujeruhiwa.
Afisa huyo Norman Mwongera amekuwa akiishi katika msitu huo wa Boni kwa siku zote 17 bila maji wala chakula, amejitokeza katika kambi ya kijeshi ya Basuba inayopakana na msitu wa Boni akiwa amedhohofika kiafya.
Idara ya ulinzi nchini KDF imemsafirisha Mwongera kwa ndege hadi jijini Nairobi ili kupata matibabu ya dharura huku akiwa na majeraha ya risasi mkononi na kwenye bega.
Mwongera alikuwa na bunduki yake sawia na bastola iliyokuwa ingali na risasi, na amekuwa katika msitu wa Boni ambao ni kambi ya wanamgambo wa Al-shabab kwa muda sasa.
Hata hivyo, katika tukio hilo la mapema mwezi Mei mwaka huu, idara ya ulinzi nchini KDF ilikanusha kwamba kuna baadhi ya Maafisa waliyofariki katika mkasa huo wala kupotea ikisema Maafisa wote waliyohusika katika mkasa huo walipatikana.