Afisa wa kitengo cha dharura katika Shirika la utetezi wa haki za kibinadamu nchini MUHURI Francis Auma ametiwa nguvuni na kuzuiliwa kwa muda katika kituo cha polisi cha Makupa mapema hii leo.
Auma aliyekwenda kituoni humo kufuatilia kesi inayofungamana na unyanyasaji dhidi ya binadamu amedai kuzabwa makonde na Afisa mmoja wa polisi na kumzuiliwa kwa muda.
Akizungumza baada ya kuachiliwa huru, Auma amekosoa hatua hiyo akisema kwamba Maafisa wa usalama wanapaswa kuwatendea haki na kuwahudumia wananchi bila ya kuwahangaisha.
Auma amezitaja huduma za Maafisa wa usalama katika kituo hicho kama zinazodidimia akiitaka mamlaka ya IPOA kuidhinisha uchunguzi wake kuhusu utendakazi wa Maafisa wa polisi katika kituo hicho.