Mzazi mmoja aliye na mwanafunzi katika shule ya msingi ya St. Claret huko kiembeni Kaunti ya Mombasa anataka mwanawe apate haki baada ya kujeruhiwa vibaya sikio na mwalimu wa shule hiyo.
Mamake mtoto huyo Caro Rita amesema kwamba Mwalimu wa shule hiyo aliyefahamika kama Muindi Maina Abiud alimfinya sikio lake la kushoto msichana huyo wa darasa la sita na aliye na umri wa miaka 10 na kumjeruhi vibaya sana.
Kulingana na Rita, walimu wa shule hiyo iliyo chini ya Kanisa katoliki jimbo la Mombasa, wamekuwa wakimhangaisha na kumkejeli mwanawe kufuatia hatua ya mzazi huyo kuwasilisha lalama zake katika kituo cha polisi.
Rita hata hivyo amesisitiza kwamba kamwe hatalegeza kamba hadi mwalimu huyo aadhibiwe akisema kwamba huenda shule hiyo inawadhulumu mno Wanafunzi.
Tayari mwalimu huyo amefikishwa mahakamani na kuwachiliwa kwa pesa taslimu shilingi elfu tano.
Kwa upande wao, Afisa wa maswala ya dharura katika Shirika la utetezi wa haki za kibinadamu nchini MUHURI Francis Auma na mwenzake wa maswala ya jinsia na haki za watoto Bi Topista Juma wameitaka wizara ya elimu kuingilia katika na kuchunguza shughuli katika shule hiyo.
Auma amesikitishwa na tukio hilo akisema kwamba ni lazima uchunguzi wa kina ufanywe na wahusika wote wakiwemo wasimamizi wakuu wa shule hiyo kuadhibiwa kutokana na dhuluma hizo zinazotekelezwa ndani ya kanisa.
Taarifa na Gabriel Mwaganjoni.