Story by Gabriel Mwaganjoni –
Mahakama mjini Voi imemuachilia huru Mwakilishi wa Wadi ya Sagalla Godwin Kilele baada ya kiongozi huyo kukabiliwa na mashtaka ya uchochezi.
Kabla ya Mahakama hiyo kutoa uamuzi wake, Mahakama ilielezwa kwamba mnamo tarehe 12 ya mwezi Disemba mwaka wa 2019, Kilele alitoa matamshi kwamba ni sharti Shirika la uhifadhi wa wanyama pori nchini KWS kuwahifadhi ndovu ndani ya mbuga za wanyama za Tsavo Mashariki na Tsavo Magharibi la sivyo jamii ichukue jukumu la kuwaangamiza ndovu hao.
Hakimu wa Mahakama ya Voi Fredrick Nyakundi amesema Kilele hana makosa yoyote kwani alikuwa analishinikiza Shirika la KWS kuchukua jukumu lake na kusitisha uzembe kwa kuwatelekeza ndovu hao.
Nyakundi amesema ni lazima Shirika hilo liwalinde wakaazi wa kaunti ya Taita Taveta dhidi ya uvamizi wa wanyama pori hasa ndovu ambao wamekuwa wakiyavamia mashamba yao na kuharibu mimea sawa na kuwauwa baadhi ya wakaazi wa kaunti hiyo.
Kilele amekumbatia uamuzi huo akisema kumekuwa na mgogoro wa muda mrefu kati ya wakaazi na wanyamapori katika kaunti ya Taita taveta huku Shirika la KWS likichukua miaka mingi katika kuwafidia waathiriwa.