Story by Mwanaamina Fakii:
Gavana wa kaunti ya Kwale Salim Mvurya amewakosoa wahudumu wa Afya katika kaunti hiyo ambao wanaendelea na mgomo licha ya kulipwa mishahara yao.
Akizungumza katika hospitali ya Kwale baada ya kushuhudia zoezi la kupeana chanjo ya Corona kwa wakaazi wa Kwale, Mvurya amesema licha ya serikali yake kufanya kikao na viongozi wa chama cha wahudumu wa afya kuhusu kulitatua tatizo hilo bado wahudumu hao wamedinda kurudi kazini.
Akigusia swala la kupandishwa vyeo kwa wahudumu wa afya, Mvurya amesema serikali yake iko na mfumo maalum wa kupandisha vyeo wafanyikazi na tayari zaidi ya wahudumu wa afya 300 wamepandishwa vyeo.
Wakati uo huo amedokeza kwamba serikali ya kaunti imeiandikia barua chama cha wahudumu wa afya nchini, kuwataka wahudumu wa afya kurudi kazini ili kuwahudumia wananchi.