Story by Gabriel Mwaganjoni-
Muungano wa ‘One Kenya Alliance’ umevikashfu baadhi ya vyombo vya habari nchini kwa kuangazia visivyo mkutano wa Muungano huo na Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Mombasa uliaondaliwa siku ya Jumatano.
Kulingana na mmoja wa vinara hao Musalia Mudavadi ambaye pia ni Kinara wa Chama cha ANC, muungano huo haujaafikia lolote kuhusu kumuunga mkono mgombea yeyote, hivyo basi taarifa ambazo zimekuwa zikiendelezwa ni uvumi mtupu.
Akiwahutubia Wanahabari katika hoteli moja kaunti ya Mombasa, Mudavadi amesema Muungano huo ungali katika majadiliano ya kina na Vinara wengine na hakuna maafikiano yoyote.
Mudavadi amewataka wakenya kuzipuuza taarifa hizo na badala yake kusubiri muongozo sahihi kutoka kwa vinara wa muungano huo na wala sio uvumi kutoka kwa baadhi ya vyombo vya habari.
Hata hivyo inadaiwa kwamba Rais Uhuru Kenyatta hivi karibuni aliwarai viongozi hao akiwemo Musalia Mudavadi wa chama cha ANC, Kalonzo Musyoka wa Wiper, Moses Wetangula wa Ford-Kenya na Gedion Moi wa KANU kumuunga mkono Kinara wa Chama cha ODM Raila Odinga katika kampeni za kuingia Ikulu mwaka wa 2022, madai ambayo vinara hao wameyapuuzilia mbali.