Story by Mimuh Mohamed-
Kamati ya bunge la Seneti kuhusu ugatuzi na uhusiano mwema kati ya serikali kuu na zile za kaunti, imemtoza faini ya shilingi laki tano Inspekta Jenerali wa polisi nchini Hillary Mutyambai kwa kukwepa vikao vya kamati hiyo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang, amesema licha ya Mutyambai kuagizwa kufika mbele ya kamati hiyo kuhojiwa amekwepa vikao vya kamati hiyo mara tatu mfululizo.
Kwa upande wake Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen ambaye pia ni Mwanachama wa kamati hiyo amesema ni lazima Mutyambai ambatanishe ushahidi wa kuonyesha kwamba faini hiyo ya nusu milioni ameilipa kutoka kwa akaunti yake ya kibinafsi na wala sio kutoka mfuko wa serikali.
Mutyambai alitakiwa kufika mbele ya kamati hiyo kuhojiwa kuhusu suala la kufurushwa kwa wakaazi wa nyumba za Pumwani na Eastleigh jijini Nairobi, zoezi ambalo liliongozwa na maafisa wa polisi na wale wa NMS.