Story by Our Corresponents-
Wagombea wote wa urais ambao wameidhinishwa na Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC sasa serikali itawapa maafisa kumi wa usalama ili kulinda.
Inspekta Jenerali wa polisi nchini Hillary Mutyambai amesema tayari idara ya usalama imetenga jumla ya maafisa mia mbili wa usalama kutoka vitengo mbali mbali vya usalama ikiwemo wa GSU na magereza wa kuwalinda wagombea wa urais.
Maafisa hao wa usalama wataanza rasmi majukumu yao punde tume ya IEBC itakapo chapisha katika gazeti rasmi la serikali majina ya wagombea wa urais na wagombea wenza wao mnamo siku ya Jumatano jumahili.
Kulingana na sheria, wagombea wa urais pamoja na wagombea wenza wao wanapaswa kulindwa muda wote na maafisa wa usalama na maafisa hao watalinda pia afisi na nyumba zao kipindi chote cha kampeni hadi wakati wa uchaguzi.
Kutokana na hitaji hilo la sheria katika kipindi hiki cha miezi miwili cha kampeni, wagombea wa urais na wagombea wenza wao watazuru kila pembe ya taifa hili wakiwa na walinzi watano huku walinzi watano waliosalia wakilinda makaazi yao yaliopo mijini na mashambani.