Story by Mimuh Mohamed–
Huku wadau mbali mbali wakiendelea kusherekea wanafunzi waliofanya vyema katika mtihani wa KCSE wa mwaka 2021, ukanda wa pwani umejizolea sifa baada ya mwanafunzi bora wa kike katika mtihani huo kutoka Pwani.
Katika matokeo yaliotangazwa siku ya Jumamosi, Waziri wa elimu nchini Prof George Magoha alisema mwanafunzi wa shule ya upili ya Kenya High Muendo Cicily Mutheu kutoka kaunti ya Kwale aliorodhesha matokeo bora kwa wasichana na kushikilia nafasi ya sita kitaifa kwa kupata alama ya A ya pointi 87.
Katika mahojiano ya kipekee na meza yetu ya habari, Mutheu anayepania kuwa mhandisi ameelezea furaha yake baada kuorodhesha matokea bora huku akiwashauri wasichana wenza kuzingatia masomo.
Kwa upande wake Joel Mutonga ambaye ni babake mwanafunzi huyo amesema nidhamu ya hali ya juu ya mwanawe pamoja na bidii shuleni ni kati ya mambo yaliomfanya kupata matokeo ya kuridhisha.
Vile vile wasichana wengine wawili kutoka eneo bunge la Malindi kaunti ya Kilifi, akiwemo Lucy Defano na Veronica Agunga wameuletea sifa ukanda wa pwani kwa kuwa miongoni mwa watahiniwa wa kike waliopata alama bora kitaifa.
Lucy Defano ambaye amesomea shule ya upili ya wasichana ya Moi mjini Eldoret amepata alama ya A, huku Veronica Agunga wa shule ya wasichana ya Loreto mjini Limuru akipata alama ya A- mtawalia.
Katika mtihani huo wa KCSE wa mwaka 2021 ni wanafunzi 1,138 waliopata alama ya A kati ya wanafunzi zaidi ya laki 8 waliofanya mtihani huo.