Story by Mercy Tumaini-
Mbunge wa Rabai Antony Kenya Mupe amewashauri wazazi wa eneo bunge hilo kutumia lugha nzuri wanapowarekebisha watoto wao wakati huu wa mitihani ya kitaifa ili kuwapa mazingira bora ya kufanya mitihani.
Kiongozi huyo amesema hatua hiyo itachangia watoto kuorodhesha matokeo bora zaidi kwani kutakuwa na ushirikiano bora baina ya mzazi na mtoto nyumbani sawa pamoja akiwa shule akiendelea na mtihani wake.
Akizungumza wakati wa zoezi la ugavi wa chakula cha msaada kwa watahiniwa wa shule za msingi za eneo bunge la Rabai, Mupe amesema atahakikisha watahiniwa wote katika eneo bunge hilo wanapata chakula.
Kwa upande wao walimu wakiongozwa na Josephine Ngaji kutoka shule ya msingi ya Bedida pamoja na wazazi wa shule za eneo bunge hilo wamesisitiza haja ya mpango wa chakula shuleni kuendelezwa kufuatia changamoto wanazopitia wazazi.